Magreth hakusita alianza kumueleza mwanzo wa mahusiano yao yeye na Jonathan mpaka sasa.“Kwa hiyo namchukia sana huyo mwanamke natamani nimjue kwani kila siku nikimuuliza Jonathan kuhusu malengo yake na mimi hataki kuwa muwazi anaishia kuniambia kuwa anampenda sana huyo mwanamke.

 

 

“Natamani nimjue huyo mwanamke na sasa hivi nimeanza kumkera ninachokifanya ninatunga ujumbe mbaya katika simu unao onyesha Jonathan anatoka na mwanamke mwingine kisha namtumia ilimradi tu niyavunje mahusiano yao, simpendi huyo mwanamke ningekuwa nina uwezo ningemuondoa duniani ilimradi tu niwe na Jonathan,” Magreth alimalizia kuongea.

 

Abigail alivuta pumzi kwa nguvu na kuitoa nje kisha aliuvaa ujasiri. “Enhee! inaonekana unampenda sana Jonathan, unaweza kunionyesha huo ujumbe unaoutengeneza na kumtumia huyo mwanamke ili kuyavunja mahusiano yao?” Alihoji Abigail.

 

“Ndiyo, huu hapa,” Magreth alimuonyesha. Ulikuwa ni ule ujumbe ambao aliwahi kuupokea kwa namba ngeni akiwa ofisini. “Kumbe huyu ndiye yule dada aliyenitumia ujumbe ulee!?” Abigail aliwaza.

 

 

“Anhaaa…sawa, kwa hiyo yeye ana malengo gani na huyo mwanamke ama kila siku anakwambia anampenda tu?” Aliuliza Abigail. “Binafsi nashindwa kumuelewa kwani kila nikimuuliza malengo yake juu yangu, huwa haniambii huishia kusema kuwa bado anampenda sana huyo mwanamke.” Alijibu Magreth.

 

Abigail alicheka kwa kejeli kisha alimuaga Magreth. “Magreth siku nyingine tukionana nitakueleza kuhusu mimi, kwa leo naomba niwahi kwani nahitajika kazini sasa hivi,” Abigail aliondoka akiwa ni mwenye mawazo mengi sana, aliendesha gari kwa kasi kuelekea nyumbani kwake Felix.

 

 

“Kumbe huyu ndiye yule mwanamke aliyenitumia ule ujumbe! Na kwa nini Jonathan ananiambia kuwa huyu mtoto siyo wake? Na Felix ananiambia huyu mtoto ni wake? Kuna nini hapa mbona navurugikaaa!” Abigail aliwaza na kujikuta akiupiga piga usukani wa gari kwa nguvu.

 

Baada ya kufika kwa Felix alishuka ndani ya gari na kumshika mwanae mkono alimvuta haraka haraka huku wakielekea ndani. “Ni bora nimekukuta Felix, leo hukwenda kanisani kumbe! Sasa nataka uniambie vizuri ile stori ambayo ulitaka kuniambia ya kuwa huyu mtoto ni wako,” Abigail aliongea huku akihemea juu juu. “Mbona unahema hivyo? Ulikuwa wapi na mbona umefika na kuniuliza swali hilo kwani kuna nini?” Felix alihoji.

 

 

“Hapana hakuna shida si unajua leo ni Jumapili hakuna foleni ya magari, kwa hiyo nimekuja naendesha gari kwa kasi na istoshe kipindi nipo njiani nilikumbuka ile siku uliyoniambia kuwa huyu mtoto ni wa kwako. Sasa nataka nijue ilikuwaje akawa wako?”

 

 

Alijibu Abigail huku akionyesha kutabasamu kwa mbali. “Sawa nitakueleza ila naomba uniahidi kuwa haitakuwa kikwazo katika maandalizi ya ndoa yetu,” alijibu Felix. “Nakuahidi sitaivuruga mipango yetu ya harusi,” Abigail aliahidi na kisha Felix akawa huru kumsimulia ukweli kuhusu mtoto Elizabeth.

 

 

“Mimi na Jonathan tulikuwa marafiki wa karibu sana, tangu tukiwa shuleni na hata baadae tulibahatika kukutana katika uwanja wa biashara. Tulifanya biashara pamoja kiasi cha kuaminiana sana na ilifikia kipindi kila mmoja akampa mwenzake uhuru kwenye biashara yake. Kama sipo, Jonathan aliweza kusimamia biashara zangu na kama yeye hayupo pia niliweza kusimamia biashara zake.

 

 

“Siku moja nikiwa nimetoka safari, Jonathan alinipigia simu akinihitaji niende nyumbani kwake. Sikusita niliukubali wito wake. Baada ya kufika nyumbani kwake, hakupoteza muda alianza kunieleza alichoniitia. Aliniambia kuna binti ametokea kumpenda sana ambaye ni wewe Abigail.

 

 

Akaniambia angependa ampatie ujauzito ili iwe sababu ya yeye kumuoa haraka kabla hajachumbiwa na mwanaume mwingine,” Felix aliweka nukta kisha alivuta pumzi na kunyamaza kwa sekunde chache kisha aliendelea:

 

 

“Sikuamini kile alichokisema kwani nakumbuka tukiwa shule alipenda kuniambia anachukia sana kuzaa nje ya ndoa. Sikutaka kumkumbusha hilo nilimuacha anielezee mpango wake mzima. Alihitaji huo mpango wake wa kukupatia ujauzito ukamilike haraka iwezekanavyo na baada ya kujifungua basi mfunge ndoa, lakini cha kushangaza zaidi, alitaka mpango huo niukamilishe mimi na….” kabla Felix hajamaliza, Abigail alidakia.

 

 

“Huo mpango uukamilishe wewe!? Ebu kuwa siriasi na unachoniambia hapa,” “Abigail umetaka nikueleze ukweli, sasa kwa nini usitulie na kuendelea kunisikiliza nimalizie na ujue kuwa ni kweli Elizabeth ni mwanangu halali,” alijibu Felix na Abigail akakubali kuwa na utulivu kisha Felix aliendelea kumsimulia kilichotokea.

 

 

“Nilipomuuliza sababu ya yeye kufanya hivyo aliniambia kuwa, ana tatizo la ‘Azoospermia’ yaani hakuwa na uwezo wa kumpatia mwanamke ujauzito na tatizo hilo aliligundua baada ya kuishi na mwanamke kwa muda wa miaka miwili bila mwanamke huyo kupata ujauzito na walipokwenda hospitalini kupima iligundulika kuwa tatizo lipo kwake Jonathan.

 

 

Kiukweli nilisikitika sana kuujua ukweli huo na siku hiyo nilimkatalia ombi lake. Tuliagana na nikaondoka japo hakuacha kuniomba nimtimizie haja yake kwani aliendelea kunisumbua na kunisisitiza nifanye hivyo.

 

 

“Nakumbuka siku moja alinitumia ujumbe mfupi kwenye simu yangu. “Tafadhali rafiki yangu naomba unisaidie nakuahidi kukupa pesa yoyote utayoitaka endapo utanitimizia hili.” “Ilifikia kipindi nikaanza kumuelewa. Siku moja tulikutana ofisini kwangu na kuanza kupanga jinsi ambavyo tungeufanya mpango huo na kiasi cha pesa ambacho angenipatia endapo ningeukamisha mpango wake.

 

 

“Aliniambia endapo nitakupa ujauzito na ukazaa mtoto wa kiume, basi angenipatia milioni 10 pesa taslimu za Kitanzania. Lakini ikitokea nikikupa ujauzito na ukazaa mtoto wa kike basi asingeweza kutoa pesa yoyote. Alitaka uzae mtoto wa kiume ili apate mrithi wa mali zake.

 

 

Alimtafuta daktari bingwa wa maswala ya uzazi ukatupa utaratibu mzima wa jinsi ya kufanya ili azaliwe mtoto wa kiume. Kitendo hicho kilinipa ujasiri na uhakika kuwa ni kweli nitamtimizia haja yake na angenipatia malipo yangu kama alivyoahidi. Nilipomkubalia tu ombi lake, alianza kuandaa mazingira ya mimi na wewe kukutana pasipo wewe kujua na kisha niukamilishe mpango huo pasipo wewe kujua pia.

 

 

“Ilikuwa Jumamosi usiku alinipigia simu na kuniambia kila kitu kipo tayari na hivyo niende kwake kwa ajili ya kuukamilisha mpango huo. Sikuchelewa niliwasha gari langu na ndani ya dakika chache tu nilikuwa nimewasili kwake.

 

 

Nilipoingia ndani aliniambia nipitilize moja moja chumbani kwake. Nilistaajabu kukuona ukiwa umelala fofofo kitandani na ukiwa umevalia kanga moja tu. Niliogopa sana nilihisi ungeshituka kutoka usingizini na kugundua kilichokuwa kinaendelea.

 

 

Nilipomuomba anihakikishie kama usingeshituka, aliniambia huwezi kushituka wala kuamka kwani ulikuwa kwenye usingizi mzito sana ambao ungekuchukua zaidi ya masaa tano pasipo kushituka. Alisema alikupatia juisi ambayo ndani yake aliweka dawa ya kukufanya upate usingizi mzito. Alizima taa kisha aliniambia, “Felix kazi ni kwako hakikisha huniangushi,” Nikamwambia nitajitahidi.

 

 

Felix alishindwa kuendelea kusimulia kwani Abigail alianza kulia mpaka macho yake yalibadilika rangi na kuwa mekundu kabisa. Hakuwahi kufikiria kama Jonathan angeweza kumfanyia kitendo kama hicho. “Abigail mpenzi, nyamaza najua hii taarifa inaumiza lakini sina jinsi inanibidi nikueleze kila kitu unielewe,” Felix alimbembeleza Abigail kisha aliendelea kumueleza kisa kizima.

 

 

******************ITAENDELEA*********************