8 Februari 2021, 06:43 EAT
Rais wa Marekani Joe Biden anasema hataondoa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran hadi itakapotimiza makubaliano yaliyofikiwa chini ya mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015.
Bw Biden alikuwa akizungumza na shirika la habari la Marekani CBS News la Marekani, kwenye mahojiano yaliyotangazwa Jumapili.
Lakini kiongozi wa ngazi ya juu zaidi wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amesema Tehran itarejea tu kwenye utekelezajiwa wa makubaliano hayo kama Marekani itaondoa kwanza vikwazo vya kiuchumi dhidi yake.
Mkataba wa mwaka 2015 ulilenga kuweka ukomo wa mpango wa nyuklia wa Iran, iwapo ingetaka kulegezwa kwa vikwazo hivyo.
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, hatahivyo, aliiondoa Marekani katika mkataba huo mwaka 2018 na kuiwekea tena vikwazo, na hivyo kuifanya Iran kuacha kutekeleza baadhi ya ahadi zake katika mkataba huo.
Iran, ambayo inasema kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa amani, imekuwa ikiendelea kuongeza kiwango chake cha ururubishaji wa madini ya uranium. Madini ya uranium yaliyorutubishwa yanaweza kutumiwa kutengeneza mabomu ya nyuklia.
Ni kwanini mkataba wa nyuklia ulivunjika ?
Chini ya makubaliano ya mkataba wa mwaka 2015 - mapatatano yaliyofikiwa baina ya Iran, Marekani, Uchina, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Uingereza - Serikali ya Tehran ilikubali kupunguza urutubishaji wa madini yake ya uranium na kuwaruhusu wakaguzi w akimataifa kuyafikia maeneo na viwanda vya urutubishaji wa madini hayo.
Na kwa kutekeleza hilo, vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Tehran viliondolewa,
Lakini Trump aliiondoa Marekani kwenye mkataba huo unaofahamika kama -Mpango wa pamoja wa kina wa utendaji- (JCPOA), katika jitihada za kuishurutisha Iran kufanya mazungumzo ya mkataba mpya, na akarejesha tena vikwazo vya kiuchumi dhidi yake.
Bw Trump alitaka kuzuia kabisa mpango wa nyuklia wa Tehran na pia kuzuia utengenezaji wake wa makombora ya masafa marefu ya ballistic.
Iran ilikataa . Mwezi Julai 2019, ilikiuka 3.67% ya kiwango cha urutubishaji wa madini ya uranium kilichokuwa kimekubaliwa na Januari mwaka huu ilitangaza kuwa imefufua tena urutubishaji wa uranium kwa 20%- kiwango cha uranium kinachotengeneza silaha ni 90%.
Katika video fupi ya sehemu ya mahojiano iliyochapishwa kabla ya mahojiano kamili Jumapili, Bw Biden aliulizwa iwapo ataondoa vikwazo vya kiuchumi ili kuieta Iran tena kwenye meza ya mazungumzo, na jibu lake lilikuwa ni ''Hapana''
Wakati huohuo, Ali Khamenei alisema kwamba kwa Iran kurejea katika utekelezaji wa ahadi zake chini ya mkataba , Marekani sharti kwamba "Ifute vikwazo vyote ", iliripoti televisheni ya taifa la Iran siku ya Jumapili.
"Tuta tathmini, na kama tutaona kwamba wamechukua hatua za uaminifu katika suala hili, tutarejea tena kutekeleza ahadi zetu," alisema na kuongeza kuwa: " Hatuwezi kujbadilisha msimamo huu na ni uamuzi wa mwisho na maafisa wote wa Iran wamekubaliana kuuhusu"
Biden alisema nini kingine?
Rais Biden pia alizungumzia kuhusu mahusiano ya Marekani na Uchina.
0 Comments